PADRI KARUGENDO ACHA VIONJO!
Mwanafalsafa wa siku nyingi Permanides anatuasa juu ya ukweli anasema watu wanachanganya kati ya ukweli kadri unavyojitokeza kwao-relative truth na ukweli halisi-objective truth anasema ni vizuri kuangalia kitu kama kilivyo na si-vinginevyo,hii ilimfanya mwanafalsafa Plato kuugawa ulimwengu katika makundi mawili,yaani ulimwengu wa busara na akili-intelligible world na ulimwengu wa mwonekano-sensible world na kadiri ya Plato wale wenye busara na fikara sahii wapo kwenye ulimwengu wa ukweli na wale wenye vionjo wapo kwenye ulimwengu wa maoni/maono!
Hivyo katika kutoa hoja zetu ni vyema tufuate taratibu za fikara sahihi na si-vionjo kama Karugendo!
Makala aliyojibu Padri Privatus Karugendo ya jumapili 25,Febr 2007,ISSN 0856-9762 Na.814 katika gazeti hili la Tanzania Daima yenye kichwa cha habari “Sijapotoka ni maoni!” inaonyesha mambo makuu mawili mosi Karugendo bado hajaelewa kwa kina kuhusu kondomu,ukimwi,na sakramenti ya kitubio! Pili Karugendo anashindwa kutofautisha kati ya ukweli kadri unavyojitokeza kwake na ukweli ulivyo na hili ni tatizo la wengi!Binafsi sitachoka kumwelimwisha babu yangu na matumaini ya kumpata yapo!
Ukisoma kwa makini katika makala zile mwandishi “amejifunua” na binafsi nimepata faida ya kumjua ni nini anachowaza! Na ndio maana leo namwambia aache vionjo/maoni afuate ukweli ninaomweleza!
Simkatazi siku nyingine kutokuandika maoni yake la hasha! Unapoandika maoni ni sawa na mvuvi anayetupa ndoana mtoni! Maoni ni njia ya kuupata ukweli na unapopewa ukweli haraka uufuate, namwambia sasa afuate ukweli na awe muumini wa ukweli kondomu,kitubio,na ukimwi!
Mwandishi anasema amefanya kazi ya upadre kwa miaka 17 hivyo anaelewa anachozungumza na mimi kama mjukuu niache opium! Hii inanifanya nicheke kidogo! Hapa kuna maswali najiuliza kwa kuwa karugendo amefanya kazi ya upadri kwa miaka 17 na kwa mujibu wa mafundisho tunaambiwa mapadri huishi useja,je yeye karugendo alifuata maadili? Na kama Alifuata kwa nini anasema watu hawawezi kuacha ngono kabla ya ndoa? Na kama hakufuata je anafikiri sababu ya yeye kushindwa kuuishi useja wake ni sawa kwa watu wote? Ni sababu zipi zilizomfanya ashindwe? Je alitumia kitubio na akashindwa kujizuia?
Pia naona mwandishi amepotoshwa na methali ya kiswahili isemayo “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu” napenda aelewe kwamba ni kweli mimi ni mjukuu wake kiumri! Si kiuelewa wa mada hii! Hivyo methali yake haina uhusiano kabisa.
Asiyesikia la mkuu huvunjia guu maana yake ni kwamba asiye sikiliza la msema kweli juu ya jambo fulani ilhali yeye ama hajui au ana elimu ndogo basi mtu huyo ni rahisi sana kupata madhara kwa baadaye! Karugendo kwa vile amesema anatoa maoni basi yeye ndiye mjukuu kwa maana ya uelewa wa suala hili hata kama ameandika kuhusu ukimwi tangu 1997 hilo halijalishi! Pili akumbuke kuwa “ukubwa wa pua si-wingi wa kamasi”
Mwandishi anasema hata Yesu akija leo hii atakaa na wanaotetea kondomu kwani alikaa na mafarisayo,malaya na wengineo! Kwa kuwa Yesu ni mwalimu wa wanaoitafuta kweli ni kweli kabisa atakaa na wote anaowataja mwandishi!
Kisha Yesu atawauliza Ninyi ni akina nani? Ni nini shida yenu hasa mpaka mkatengeneza kondomu? Kwa nini hamjafikiria juu ya kuwafundisha watu kuacha kufanya ngono? Mnajua kama ninyi ndio ma-CEO/GMs wa hapa duniani? Kwa nini mnaitia dhambi manukato? Mbona mnakana cheo chenu na mnajiita wajasiriamali wa kondomu? Kama mmeshindwa je mmemuuliza Baba yenu aliye mbinguni? Amesemaje?
Yesu akiwa anawauliza maswali haya wataangaliana wao kwa wao na kuanza kunyoosheana vidole! Yesu atawaambiwa yaliwapasa muwe na akili ya uchaji si ya kibinadamu! Nendeni mkatengeneze bustani na kurudisha heshima ya tendo la ndoa duniani! Mkifanya hivyo baba yenu atawasamehe na mtatimiliza azma yake katika ulimwengu huu! Kisha yesu atawatoka!
Karugendo ameshindwa kutofautisha kati ya dhambi na mtenda dhambi! Kwa kadiri ya mafundisho yatupasa kutowachukia watenda dhambi ila dhambi! Na Yesu anaongea na wote hususani wenye dhambi,hawezi kukataa kukaa na kuwaelimisha watenda dhambi!(kwa maana nyingine Yesu hawezi kuitetea dhambi!)
Na ni kweli kwamba sisi sote ni watoto wa Mungu na wajasiriamali wa kondomu nao wataitwa watoto wa mungu lakini kuna tofauti kubwa sana kati ya watoto wa mungu na watoto wanaomtii Mungu!
Kuitwa mtoto wa mungu ni “offer” ukikubali na kumtii mungu ni “contract” na utaitwa mtoto mtiifu wa mungu Kwa hiyo watengenezaji na wapiga debe wa kondomu kama karugendo kazi kwao ama waikubali(accept) au waikatae(reject).Offer hii ipo muda wote kadri wao watakavyoishi ila wakumbuke kuwa “Killing time is not murder its suicide” soma (Yn 12:23-27,Yn 7:3-6,Yn 4:1-42,Yn 17:1-5,Efe 5:15-16,Yn 2:1-4,-NKJV)
Wajasiliamali wa kondomu kama babu yangu Karugendo ni mfano mzuri wa watu wanaopotosha umma kwa kusema eti Mungu ameasisi Kondomu,nasisitiza NI UPOTOSHAJI MKUBWA JAMANI TUSIKAE KIMYA!
Katika makala zangu za toleo 800 na 807 nilisema lengo la kitubio ni kurudisha urafiki uliopotea kati ya binadamu na Mungu wake na nikasema maungamo ya kweli ni yale yanayoendana na urekebishaji wa tabia,pia nikasisitiza kama mtu atarudia dhambi eti kisa kuna Mungu atamuondolea dhambi huyo atakuwa anamjaribu bwana Mungu wake!
Hebu ngoja tuangalie “philosophy” za kondomu,kimsingi kondomu inachochea ngono! Labda utaniuliza kivipi,pakiti za kondomu tulizo nazo madukani zina picha za “ponografia” hii inachochea ngono na inakwenda kinyume kabisa na sera ya serikali ya kuzuia picha za ngono. Pili kondomu zinafanya suala la kuacha kufanya ngono lisiwepo,kwa sababu kondomu inahubiriwa sana kuliko njia nyingine!
Mathalani kondomu zinawekwa “betri” hii itamfanya mtu ajizuie kufanya ngono kweli? Nyingine zinapewa majina ya kuonyesha umwamba katika kufanya ngono mfano kondomu inaitwa DUME!
Si-hivyo tu bali kondomu zinaharibu urafiki kati ya mtu na mtu,zinaondoa heshima ya tendo la ndoa,linaharibu maadili,na mengineyo mengi.
Pili imani zetu zinatuambia TUSIZINI lakini wajasiriamali wa kondomu wanasema TUZINI! Kwa kutumia silaha! Lakini wanashindwa kujibu swali Je kama tukitumia kondomu dhambi hatutapata?
Karugendo pia ameshindwa kujibu swali langu kuhusu kutokufanya ngono nilimuuliza ni ugonjwa gani mtu ataupata kama akikaa mda mrefu bila kufanya ngono?
Mpaka sasa hakuna mwanasayansi yeyote aliyehakikisha kama kondomu inazuia ukimwi 100%,labla mimba!
Tusidanganyike kondomu sio silaha! Ngono ina nguvu kuliko kondomu! Kuna tofauti kati ya kutumia silaha na kushika silaha! Na wataalamu wanatuambia akili ya binadamu kabla na baada ya kushika silaha ni tofauti! Hivyo silaha inaishia kukuua wewe mwenyewe! Silaha inareta kiburi cha muda tu.
Takwimu za NACP za October 2005 zinaonyesha maabukizi ya ukimwi yanaongezeka maradufu kwa mikoa ya Mbeya,Dar,Tanga na Kagera! pamoja na kutumika kwa kondomu!
Mwandishi katika makala iliyopita anasema “Si kweli kwamba mimi nimenunuliwa kuandika juu ya kondomu.Si kweli kabisa maana vinginevyo maisha yangu yangekuwa ya juu sana.hizo pesa zingeonekana tu “
Haya ni maneno mazito kwa mtu kama huyu! Lakini najiuliza mbona mimi sikumtuhumu wala kuandika juu ya yeye kununuliwa kuandika juu ya kondomu!
Mwandishi anaonyesha kujishuku na hapa kunakitu! haiwezekana akaanza kutoa hoja kama hizi! Mathalani huwezi ukapita kariakoo halafu mtu akaanza tu kusema “mimi sio mwizi! Mimi si mwizi” huyo atakuwa na lake jambo! Karugendo vipi?
Inawezekana Karugendo anahudhuria sana vijisemina na viwarsha kuhusu Matumizi ya Kondomu na hii inawaafanya watu kuhisi babu kanunuliwa kuandika kuhusu kondomu sasa aache afanye vitu vingine vipadiem hivi vitamponza!
Ukimwi na ngono haviwezi kuisha kama tutakazania kondomu! Ni jukumu letu kurudisha heshima ya tendo la ndoa kwani ni tendo takatifu.
Subiri na Tosheka naye ni ujumbe usiofaa kubezwa,Karugendo yampasa aache vionjo! Na aufuate UKWELI!
Ndimi
KILLIAN E. NANGO
P.O.BOX 9192
DAR ES SALAAM
Emaili:Killijunior@yahoo.com
“Mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa PILI,taaluma ya Uhasibu katika Chuo cha usimamizi wa Fedha IFM-Dar Es Salaam.Msomaji makini wa Tanzania Daima Jumapili,na pia ni Mwanaharakati wa YUNA na TYVA”
Monday, March 19, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment